WAKATI Sheria ya Makosa ya Mtandao inaanza kutumika leo, Serikali imewahakikishia wananchi kuwa sheria hiyo haina lengo la kuwaogopesha wala kuwanyima uhuru wa kuwasiliana, bali itawalinda dhidi ya wahalifu wa mitandao.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema jana Dar es Salaam kuwa serikali haiwezi kuingilia uhuru wa watu wa kuwasiliana, bali itafanya hivyo tu kama kuna sababu ya mambo ya usalama wa taifa.
“Serikali baada ya kujiridhisha kuwa maandalizi yote muhimu ikiwemo elimu kwa umma na kujenga uelewa kwa watekelezaji wa sheria hizi yamefanyika, sasa, sheria hizi zitaanza kutumika rasmi kesho (leo) Septemba mosi.
“Kwa hivyo, natoa rai na wito kwa wananchi wote kuwa tuzingatie matumizi salama na sahihi ya huduma za mawasiliano na mtandao kwa manufaa ya kila mmoja na kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mitandao ikitumiwa vyema ina faida kubwa sana katika jamii yetu,” alisema Profesa Mbarawa. Sheria ambazo zinaanza kutumika leo ni Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, ambazo zilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali la Agosti 14, mwaka huu.
Profesa Mbarawa alisema Tanzania siyo nchi ya kwanza kutunga sheria hizo. Alisema kuna nchi mbalimbali duniani, ambazo zimetunga sheria kama hizi na alitoa mfano wa Uingereza, India, Malaysia, Uganda, Korea Kusini, Singapore, Mauritius, Marekani na nyingi nyinginezo.
Alikiri kuwa sheria hizi zimepokelewa kwa hisia tofauti kutokana na uelewa mdogo kwa wengi wetu kuhusu sheria hizi. Vilevile, ni ukweli usiopingika kuwa kumekuwa na tafsiri hasi kwa baadhi ya wananchi juu ya maudhui ya sheria hizi na kuzifanya zitafsiriwe kama kandamizi zaidi, kitu ambacho ni tofauti na dhana na maudhi ya sheria hizi.
Alisema kwa kutambua hilo, wizara yake mara baada ya kupitishwa kwa sheria hizo, ilianza kuwaelimisha wananchi kupitia vyombo vya habari na kuwa na mikutano na makundi mbalimbali ya watekelezaji wa sheria hizo ili kuwajengea uelewa, ikiwemo Jeshi la Polisi, Waendesha Mashtaka, Wachunguzi, Wapelelezi, Mahakimu na Majaji.
Alisema ili kuhakikisha kuwa usimamizi na utekelezaji wa sheria hizi unakwenda vizuri, Wizara itaendelea kuwajengea uelewa wadau mbalimbali. Alisisitiza kuwa sheria hizo ni muhimu na zina manufaa makubwa kwenye jamii haswa katika nyakati hizi ambapo matukio ya uhalifu wa mtandao yamekuwa yakiongezeka na kukosekana kwa sheria hizi kumefanya wananchi kutokuwa na mahala pa kukimbilia pale wanapokumbana na uhalifu kupitia mitandaoni.
Post a Comment