WAKATI vyama vinavyounda umoja wa upinzani (Ukawa) vikimaliza utata wa ugawaji wa majimbo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa leo atavunja ukimya kuhusu hatima yake ya kisiasa kwa kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Ukawa imewataka wagombea ubunge waliogombea nje ya mfumo wa makubaliano, kujiondoa mara moja. Hata hivyo, bado kuna majimbo matatu yenye utata ambayo wanatafuta ufumbuzi; Mwanga mkoani Kilimanjaro ambapo Chadema na NCCR-Mageuzi wote wamesimamisha mgombea, Serengeti mkoani Mara ambako Chadema na NCCR wamesimamisha wagombea na Mtwara Mjini ambapo CUF na NCCR wamesimamisha wagombea.
Katika taarifa iliyosainiwa na viongozi wakuu wa Ukawa kuhusu mgawanyo wa majimbo, viongozi hao wamesisitiza kuwa wamemaliza mgawanyo wa majimbo kwa asilimia 90 ya majimbo yote 265 ya Tanzania Bara na Zanzibar na bado machache ambayo ufumbuzi wake utapatikana hivi karibuni.
Kwa hali hiyo, umoja huo umewataka wagombea wote wa ubunge ambao vyama vyao havikuachiwa majimbo kujitoa katika nafasi hizo na kuwapa ushirikiano wale ambao wamepewa nafasi na umoja huo ili kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi mkuu.
“Ieleweke mgawanyo huu wa majimbo hautahusiana na mgawanyo wa kata za kugombea udiwani, mwongozo wa kuachiana kata ndiyo utumike katika maamuzi ya kuamua namna ya kugombea kata,” ilieleza taarifa hiyo.
Awali, baadhi ya majimbo yalikuwa na utata ambapo miongoni mwake ni Jimbo la Segerea mkoani Dar es Salaam ambalo kwa sasa ameachiwa Julius Mtatiro wa CUF, Kigamboni ambalo ameachiwa Lucy Magereli wa Chadema, Morogoro Kusini Mashariki ambalo ameachiwa Salama Awadh wa CUF.
Majimbo mengine ni Mlimba ambalo ameachiwa Suzan Kiwanga wa Chadema, Kilombero ambalo ameachiwa Peter Kibatala wa Chadema, Morogoro Mjini Marcossy Albante wa Chadema. “Inasisitizwa kuwa Ukawa ndiyo tumaini la wananchi wanyonge wa taifa letu.
Jamii imejenga imani kwa vyama vyetu kwa dhamira ya kushirikiana katika uchaguzi huu tuliyoionesha toka mwanzo, ni kigezo tosha cha wananchi kuweza kutuunga mkono katika kufanikisha malengo ya Ukawa,” ilieleza.
Umoja huo umetaka vyama vilivyo ndani yake kujizatiti katika kuhakikisha kwamba kila ngazi ya uchaguzi inawakilishwa na mgombea mmoja wa umoja wa Ukawa dhidi ya vyama vingine.
Aidha, imetaka viongozi wote wa ngazi zote na hasa za mikoa, wilaya na kata kutokuwa kikwazo cha kufikia malengpo ya umoja kwa kutanguliza malengo binafsi. Umoja huo ngazi ya taifa umewatawaka viongozi wa ngazi hizo za chini kuzingatia mwongozo wa awali uliotolewa katika mgawanyo wa udiwani.
Lengo ni kuona viongozi hao wanafikia makubaliano ya namna ya kushirikiana katika kuachiana nafasi za kugombea wakitanguliwa zaidi na kutazama maslahi ya wananchi wote.
Wakati hayo yakijiri, leo Dk Slaa atavunja ukimya kuhusu hatima yake ya kisiasa kwa kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari cha kuaminika, mkutano huo utarushwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya televisheni pamoja na redio nchini.
Dk Slaa hajaonekana hadharani tangu chama chake kilipomkaribisha na kumteua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema kwa kofia ya Ukawa. Imeandikwa na Shadrack Sagati na Katuma Masamba.
Post a Comment