Hehehe… heeeeee, heiiiya, acha nicheke miye mwana wa marehemu, sijui wazazi wangu huko waliko wako katika hali gani, nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape kivuli chake siku ya kiama.
Waweza ona nacheka ukadhani labda nimejawa na furaha, kumbe nafsi yangu imejaa karaha, imekereka kama siyo kukereheshwa.
Kuna watu wengine kwa kweli kila kitu watende wao wakitenda wenzao huwa mwao, hutaka kuicheza ngoma hata kama siyo ya kwao, upo?
Hivi inaingia akilini mama mtu mzima kutaka kuingilia ndoa ya mwanaye? Tuchukulie mfano ni wewe mama ungekuwa na mtoto wa kike, ndoa yake ikawa inaingiliwa na mzazi mwenzako ungefurahi?
Nalisema hili kwenu nyie wenye tabia hii kwa kuwa huu ndiyo mwarobaini wenye ladha chungu lakini ndani yake unapata dawa ya kutibu maradhi yako ya nyongo.
Kwa nini leo nimeamua kuyasema haya? Jamani kuna shoga yangu mmoja kanijia mikono kichwani, machozi churuchuru nikadhani labda amefiwa, alichonieleza nilibaki mdomo wazi kama siyo kupigwa na bumbawazi.
Eti, mwanaye amekuwa akiendeshwa na mkwewe kama gari bovu. Yaani mkwewe amekuwa ndiye kinara wa nyumba na mtoto wake hafurukuti wala hatikisiki.
Eti, mwanaye amekuwa akiendeshwa na mkwewe kama gari bovu. Yaani mkwewe amekuwa ndiye kinara wa nyumba na mtoto wake hafurukuti wala hatikisiki.
Kila siku mama anamwambia mwanaye ubaya wa mkewe lakini mtoto wala hajali, maneno yanaingia sikio hili na kutokea upande wa pili hasikii kitu juu ya mkewe.
Siku moja shoga yangu akapewa na mwanaye maneno makavu, kuwa hawezi kuachana na mkewe kama anavyotaka yeye, hilo likamuuma mpaka akamua kuja kuniangushia kilio.
Mmh, makubwa limao alambe mwingine wewe ukunje uso kama ngozi ya goti, leo nataka niwaeleze nyie akina mama mnaokosa kazi na kufuatilia ndoa za watoto wenu, jamani acheniii.
Hamuoni aibu, mama mkwe kuacha kazi na kuwa kiguu na njia kufuatilia ndoa za wanao kama mkia wa ng’ombe. Kwanza kwa mila na desturi za Kitanzania ni matusi kufanya hivyo.
Itaendelea wiki ijayo, ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu.
Itaendelea wiki ijayo, ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.