Mgombea urais kupitia tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo Chadema Mh Edward Lowassa amechukuwa fomu ya kugombea urais huku shughuli za kiuchumi jijini Dar es Salaam zikisimama kwa saa kadhaa ikiwemo eneo la kibiashara la kariakoo wakati mgombea huyo alipokuwa akielekea tume ya taifa ya uchaguzi kuchukuwa fomu hiyo.
Maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na viunga vyake wamejitokeza kumsindikiza mgombea huyo huku baadhi ya barabara zikifungwa na kusababisha msongamano wa magari hasa katikati ya jiji ambapo maandamano ya kumsindikiza yameanzia ofisi za CUF Buguruni kupitia barabara ya uhuru ,bibi titi ohio hadi tume ya taifa ya uchaguzi.
Mara baada ya kuwasili ofisi za tume ya taifa ya uchaguzi wafanyakazi wa ofisi zilizopo eneo hilo walionekana wakiwa na shauku ya kumuona ambapo Mh Lowassa alipowasili ofisini hapo alikabidhiwa fomu hiyo na baadae safari ya kuelekea makao makuu ya Chadema yaliyopo Kinondoni ikaanza na hapo watumiaji wa barabara zinazoingia na kutoka katikati ya jiji wakalazimika kusimama tena kwa saa kadhaa kupisha maandamano hayo.
Akihutubia hadhara ya wafuasi wa vyama vinavyounda UKAWA pamoja na wananchi waliojitokeza kumuunga mkono Mh Lowassa amewahidi vijana, mama lishe, wamachinga na waendesha bodaboda kuwa endapo watampa ridhaa ya kuwaongoza ataunda serikali ambayo itakuwa rafiki kwao na matatizo yao yatakuwa kipaumbele cha kwanza mara baada ya kumchagua.
Kwa upande wake katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema UKAWA wanataka muungano wa haki huku mwenyekiti wa NCCR-mageuzi Mh James Mbatia akiendelea kuwasisitiza wana UKAWA na watanzania kuendelea kushikamana na kuwa wamoja na wasikubali siasa iwatenganishe kwani umoja wao ndio utakaowezesha amani iliyopo hapa nchini kuendelea kudumu.
Maandamano hayo yaliongozwa na baadhi ya viongozi wanaunda UKAWA, wabunge wa vyama vinavyounda UKAWA kutoka mikoa mbalimbali nchini huku jeshi la polisi likiimarisha ulinzi tangu mwanzo wa maandamano hayo hadi walipohitimisha katika ofisi za Chadema Kinondoni.
Post a Comment