Johannesburg, Midrand
Idara ya elimu ya serikali ya Afrika Kusini kwa kushirikiana na makampuni ya Vodacom,Huawei na taasisi ya Nelson Mandela Foundation imezindua mpango wa maktaba kwa njia ya mtandao wa kidijitali lengo kubwa likiwa ni kuboresha huduma za elimu nchini humo.

Mpango huu utatekelezwa kwa kutumia programu zenye maudhui ya elimu zinazopatikana bure kwenye simu za kampuni ya Huawei zilizounganishwa na vituo vya habari na teknolojia na mawasiliano vya kampuni ya Vodacom ambavyo vimeenea nchini kote.

Huduma hii ya Huawei chini ya uwezeshwaji wa Vodacom imepakiwa vitabu vya kijigitali zaidi ya 400 vya fani mbalimbali kuanzia historia, Biashara, fasihi ya kiafrika na riwaya . Vitabu hivyo vya kidijitali vinapatikana katika lugha 11  kwa kushirikiana na makampuni maarufu ya uchapishaji vitabu ya Oxford University Press, Shuter & Shooter, FunDza  na maudhui yake yamepitiwa na kuidhinishwa na Idara ya elimu ya Afrika Kusini kwa kushirikiana na taasisi ya Nelson Mandela Foundation.
Mtendaji Mkuu wa makampuni ya Vodacom , Shameel Joosub anasema: “Lengo letu kubwa la kutekeleza mpango huu ni kuhakikisha tunatumia teknolojia kuleta mabadiliko kwenye jamii hususani kwa wateja wetu.Kupitia mpango huu tumedhamiria kuhakikisha tunawawezesha wanajamii kupata maarifa yanayopatikana kwa kusoma vitabu vilevile kuburudika na vitabu  kupitia maktaba za kidijitali bure.”

Aliongeza kwa kusema kuwa upatikanaji wa vitabu na machapisho mbalimbali ni changamoto kubwa nchini Afrika Kusini kutokana na kutokuwepo huduma nzuri za maktaba,Vodacom kwa pamoja na  taasisi ambazo imeshirikiana nazo kutekeleza mpango huu   inaamini kuwa kwa kiasi kikubwa utasaidia kuongeza maarifa na ujuzi kupitia  usomaji wa vitabu na machapisho mbalimbali kwa njia ya mtandao ."

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa kampuni ya Huawei  ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, You Jiangtao anasema: “Huawei  imekuwa ikishirikiana na Vodacom  kuboresha mawasiliano na kurahisisha maisha kupitia mtandao wa simu  na kuunganisha watu duniani kote. Tunafurahi kuwa sehemu ya mpango huu wa kuendeleza  jamii kielimu na tuna imani kuwa walengwa wataitumia fursa hii vizuri."

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela Foundation, Sello Hatang alisema kuwa Nelson Mandela alipenda kutoa kauli hii kuwa “Maisha ya mtu hayaangaliwi kwa jinsi anavyoishi binafsi bali kinachoangaliwa amejitoa kwa namna gani kusaidia watu  wengine“  na  aliongeza kusema kuwa Nelson Mandela alikuwa akiheshimika duniani kote kutokana na mchango mkubwa alioutoa wa kujitoa mhanga kusaidia watu wengine ambapo  watu wengi wanaishi maisha bora  na ndoto zao za maisha ya baadaye zimetimia kutokana na kiongozi huyo kujitoa kwa ajili ya watu wengine.
Mpango huu umepanua huduma za Vodacom kutumia mtandao wake katika kuboresha elimu kupitia njia mbalimbali baadhi yake zikiwa ni  kujiunganisha na vituo vyake vya habari na teknolojia na mawasiliano, kutumia mtandao wake wa madarasa ya kidijitali kwa interneti, mpango wa kutoa elimu kwa njia ya masafa kupitia simu za mkononi, mpango maalumu wa kutoe elimu kwa mtandao na mpango maalumu ujulikanao kama Vodacom Millionaires.

Post a Comment

 
Top