NIAlhamisi tena ambayo huwa nakutana na nyie wasomaji wangu ninaowapenda sana.Leo nataka kuzungumza na wanandoa. Ndiyo maana nimeanza kwa kusema hapo juu kuwa, ndoa isishikiliwe kama gauni la harusi.
Katika ndoa kuna raha na karaha au shida. Kumbuka kuwa wewe mwanandoa uliapa utaishi na mwenzako katika maisha yote. Hicho kiapo ulikitoa kanisani au msikitini tena kwa kuulizwa mara tatu.
Ndoa ni daraja. Kama zima unatakiwa kulivuka kama bovu pia unatakiwa kulivuka. Lakini kama ni bovu lifanyie ukarabati kwa sababu unatakiwa kuvuka.Kama nilivyoongea, katika ndoa kuna misukosuko kama lilivyo daraja bovu. Ni jukumu lako mwanandoa kuhakikisha unavuka. Ndani ya ndoa kuna vikwazo vingi, kukosa kupo, kupata ni hali ya kawaida ambayo ipo na lazima ukabiliane nayo kama ulivyoahidi siku uliyofunga ndoa.
KWA WANAWAKE WENZANGU
Kuna baadhi ya wanawake pale waume zao wanapokosa cha kusababisha uhai uendelee, basi hadi mtaa wa saba watapata taarifa. Kumbuka hakuna mkamilifu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu. Wewe mke uwe mstari wa mbele kuujua udhaifu wa mumeo kama vipi muweke chini mumeo mweleze, muongee kwa upole kabisa. Kumbuka wewe ndiyo hakimu wa nyumba yako, wewe ndiyo waziri. Unayo madaraka yote juu ya familia na mumeo kwa ujumla.
KWA WANAUME NAO
Na wewe mwanaume vilevile, ukigombana na mkeo haitakiwi siri itoke nje. Muweke kikao, mseme uwezavyo kisha myamalize. Nasema hivi kwa sababu wale unaowapelekea mashitaka, baadhi yao wana ushauri mzuri, lakini wengine ushauri wao ni mbaya hata kushauri ndoa ivunjike.
TABIA ZA WATU
Leo utachukua tatizo la mumeo unampelekea shoga. Kumbe huyohuyo shoga anamtaka mumeo. Na wewe mwanaume vilevile, utapeleka tatizo la ndoa yako kwa marafiki zako kumbe na wao wanampenda mkeo, walianza kumtamani tangu walipomuona siku ya kwanza unamuoa. Je, mtakuwa mnajenga kweli au mnajibomoa?
CHA KUFANYA
Kama kuna matatizo katika ndoa yenu, kaeni wenyewe ndani hata bila watoto kujua mmegombana myamalize kwa ajili ya kulinda ndoa yenu. Kuna wanandoa wengine hupenda kupeleka migogoro yao kwa watu wazima. Je, hamjui kama siku hizi hata watu wazima wanapenda serengeti boi? Shauri yenu!
Ndiyo maana nikasema kuwa usimpe tatizo mtu ambaye kesho na keshokutwa atakushushia hadhi na heshima yako. Hii ina maana ya kichwa cha habari kuwa ndoa usiigeuze gauni la harusi ambalo hushikiliwa na wapambe, liache liburuzike lenyewe ikibidi libebe mwenyewe.
Post a Comment