Mshambuliaji raia wa Uganda, Hamis Kiiza amethibitisha kuwepo kwa mazungumzo na klabu ya Simba na kama mambo yatakwenda sawa atajiunga na Wekundu hao wa Msimbazi majira haya ya kiangazi.
Akizungumza kutoka kwao Uganda, Kiiza amesema wakala wake amefikia hatua nzuri na Simba, hivyo wakati wowote anaweza kusaini mkataba.
"Ni kweli wakala wangu amekuwa akizungumza na Simba, ameniambia wamefikia hatua nzuri, wakimalizana kila kitu,  nitasaini Simba". Amesema Kiiza.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga amesema kama atajiunga na Simba itakuwa furaha kwake kucheza timu moja na rafiki yake Emmanuel Okwi.
"Okwi ni rafiki yangu wa siku nyingi toka tukiwa shule, tulicheza pamoja toka tukiwa wadogo, ndio maana uliona hata kwenye harusi yake mimi nilikuwa msindikizaji wake, nitafurahi kucheza naye Simba". Ameongeza Kiiza.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amethibitisha kuwepo kwa mpango wa kumsajili Kiiza na amesema kuna mambo madogo yamesalia kumsainisha mkataba.
Hans Poppe amesema Kiiza ni mchezaji ambaye anaweza kuwasaidia msimu ujao kutokana na kipaji chake na uzoefu wa soka la Tanzania.

Post a Comment

 
Top