Ndugu zangu,
Kwa mwanadamu, imani ni mtaji mkubwa sana. Anayemwamini unayemwamini nawe utamwamini. Ni asiyejua siasa tu, atakayepuuza ukweli kuwa nyuma ya Dr Slaa kuna wafuasi wake wengi wanaomwamini. Dr Slaa ni ' Celebrity Politician'- Ana wapenzi na washabiki pia, ndani ya Chadema, CCM na miongoni mwa wasio na vyama.
Dr Slaa amekuwa moja ya nguzo muhimu za siasa za upinzani hapa nchini. Kwa mtazamo wangu, njia aliyochagua kuipita sasa ni pigo kwa harakati za kujenga misingi ya siasa za ushindani wa vyama vingi hapa nchini. Si habari njema kabisa kwa wapenda demokrasia wa kweli.
Hata hivyo, Wahenga walisema; kila janga na somo lake.
Tunajifunza nini?
Ndugu zangu,
Zikiwa zimebaki takribani siku 50 tu kabla ya Watanzania kufanya maamuzi kupitia masanduku ya kura, na kwa kuitafakari kwa kina hotuba ya Dr Slaa ile jana, ni ukweli mchungu, kuwa Tanzanian opposition is in disarray- kwamba upinzani Tanzania umevurugika, hauko kwenye mpangilio. Saikolojia ya mpiga kura humwelekeza kukipigia kura anachokiamini. Wapiga kura wengi wanajua, anayempigia kura huenda ndiye atakayeunda Serikali. Wengi wa wapiga kura, na kwa nchi yetu, hutaka pia uwepo wa Stable Government- Serikali imara, hivyo, itakayohakikisha amani na utulivu wao, kwa maendeleo yao.
Tumemwona kwenye TV jana kule Masasi, Emmanuel Makaidi akikataliwa na Wananchi waliokuwa wakimtaka mgombea wa CUF. Emmanuel huyu ndiye mwenyekiti wa NLD inayounda UKAWA na anakataliwa hadharani na watu wa jimboni kwake. Na bado, katika siku 50 hizi kabla ya kwenda kupiga kura, UKAWA hawajakubaliana namna ya kugawa majimbo kwenye baadhi ya majimbo, hatujazungumzia kwenye kata za nchi hii.
Ninachokiona, shida kubwa ya upinzani ukiongozwa na Chadema ni kupoteza ajenda muhimu iliyokuwa ikiwabeba. Ajenda ya kupambana na rushwa na ufisadi. Ni ajenda waliyoikamata na wakatambulika nayo. Leo wameitupa wenyewe na kuiacha ielee. Duniani ushindi uelea, ukiupata na usipoukamata vema, ukauacha uelee, basi, kuna atakayeuchukua.
Kwenye hili la ajenda ya rushwa na ufisadi, alikotokea haijulikani, John Magufuli ameipigia mbizi na kuikamata. Na ameishikilia haswa. Nimeona kwenye matangazo ya TV akitamka kuwa " Majizi na Mafisadi Ndiyo yaliwafikisha Watanzania hapa". Magufuli anasema huku akionyesha kuichukia hali hiyo, kuwa akiingia madarakani atakwenda kuanzisha mahakama maalum itakayoshughulika na Mafisadi ili wasicheleweshe kufungwa.
Ukweli ajenda hiyo inawagusa wananchi wengi, maana ndio kero kubwa ya Watanzania. Kule Dodoma mwaka 1995, Julius Nyerere alipotamka; " Watanzania Wanataka Mabadiliko' alikuwa na maana Watanzania walihitaji kiongozi atakayewasaidia kuondokana na hali waliyokuwa nayo. Hali ya uwepo wa kero ya rushwa iliyotamalaki. Walimuhitaji kiongozi wa kuibadili hali hiyo.
Ikumbukwe, kwenye Uchaguzi wa 1995, wakati John Cheyo wa UDP alipopanda majukwaani akiwa na ajenda ya ' Kuwajaza Watu Mapesa', na akaitwa ' Bwana Mapesa', mwenzake Ben Mkapa , ambaye alikotokea haikujulikana, alikubalika haraka na alipigiwa kura nyingi na Watanzania kwa vile alipanda majukwaani mfukoni akiwa na ajenda ya kupambana na rushwa.
Na kwenye hotuba ya kwanza kabisa ya kampeni zake, Ben Mkapa alitamka; " Sitakuwa na Suluhu na Wala Rushwa!" Wapiga kura mioyoni wakasema; " Naaaam..huyu ndiye tunayemtaka aende akawashughulikie wanaotutesa". Na hakika , ni ajenda hiyo ndio iliyomwingiza Ben Mkapa madarakani.
Hivyo, kuondoka kwa Dr Slaa Chadema na Ukawa si jambo la kubeza. Dr Slaa ana ushawishi. Hiki ni kipindi ambacho, Wapiga kura walio wengi zaidi ya wanachama wa vyama vyote vya siasa, na ambao hawajafanya maamuzi, ndio wakati hujaa pia kwenye mikutano ya vyama vyote kusikiliza sera na mikakati ya kiongozi au chama husika ili waweze kufanya maamuzi. Na hapa watu wa kundi hilo watamsikiliza pia Dr Slaa.
Muhimu kwa wapanga mikakati wa Ukawa kwa sasa si kuanza ' Siasa za mipasho' na Dr Slaa, bali, ni kupambana kuzijibu hoja za Dr Slaa kwa hoja, na wakati huo huo, kujenga hoja za kuwasaidia wapiga kura ambao hawajaamua, kujibu swali la kwanini wampigie kura mgombea Urais wa Ukawa, Wabunge na Madiwani.
Maana, kwa ninavyoona, katika hali tuliyo nayo leo, kama Uchaguzi Mkuu utafanyika Jumapili hii, CCM itaibuka mshindi na kuunda Serikali.
Maggid.

Post a Comment

 
Top