ISHU! Wakati Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ikikutana leo mjini Dodoma kupitia na mwishowe kukata majina ya wagombea wanaowania kuteuliwa kwa nafasi ya Urais katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, presha ya muigizaji Jacob Stephen ‘JB’ imepanda, kwa hofu ya kutokea tafrani miongoni mwa wanachama wa chama hicho.
Akizungumza na gazeti hili juzi, JB ambaye ni kada wa chama tawala, alisema tofauti na miaka ya nyuma alipokuwa akitambua wazi nani atachukua nafasi hiyo, safari hii hali ni ngumu na kama CCM haitakuwa makini, ipo hatari ya kutokea mgawanyiko mkubwa utakaosababishwa na kukatwa kwa baadhi ya wagombea.
“Wakati Benjamin Mkapa akiwa madarakani, nilifahamu kwamba atakayefuata ni JK (Jakaya Kikwete), lakini hali ya mwaka huu ni tofauti kwa sababu haujui nani atafuata. Kwa sababu hiyo ipo haja, tena ya makusudi kabisa kuhakikisha umakini wa hali ya juu unachukuliwa katika kila hatua, vinginevyo inaweza kuleta matatizo makubwa,” alisema muigizaji huyo mkongwe akiuzungumzia mchakato huo.
Kamati Kuu (CC-CCM) itaanza kikao chake cha kuchuja majina ya wagombea hao wapatao 37 waliorejesha fomu, ili kupata majina matano yatakayopelekwa mbele ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) inayotarajiwa kukutana kesho, ambayo nayo itawakata wawili kati yao ili watakaobaki waende kupigiwa kura kwenye Mkutano Mkuu utakaofanyika kwa siku mbili za Jumamosi na Jumapili hii.
Post a Comment